Kuvunja Vikwazo: Safari ya Pendo Katika Kukuza Uongozi wa Wanawake Vijijini


Kuvunja Vikwazo: Safari ya Pendo Katika Kukuza Uongozi wa Wanawake Vijijini

By Deogratius Temba

March 26, 2025


Na Deogratius Koyanga

Iramba, Singida

“Nilizunguka nyumba kwa nyumba, nikiwaelimisha wanaume waunge mkono wanawake katika uongozi. Nilienda kwenye vijiwe vya kahawa, vilabu vya pombe za kienyeji na viwanja vya mpira sio kwa ajili ya kampeni yangu, bali kubadili mitazamo.”
Pendo Makala Mkumbo

Katika kijiji cha Mbelekese, wilayani Ikungi, mkoani Singida, mapinduzi ya kimyakimya yanaendelea. Ni mapinduzi yanayoongozwa na dhamira, ushawishi na ari ya mabadiliko kutoka kwa wanawake waliopata mafunzo kupitia mradi wa UKIJANI, unaotekelezwa na HELVETAS Tanzania. Mojawapo ya simulizi zenye kuvutia na kuhamasisha kutoka katika mradi huu ni ya Pendo Makala Mkumbo, kiongozi shupavu na mwanaharakati wa haki za wanawake ambaye amejitokeza kuwa chachu ya mabadiliko ya kijamii na kisiasa.

Kwa mujibu wa mila na desturi za jamii ya Wanyiramba, wanawake mara nyingi huchukuliwa kuwa hawafai kuongoza. Mtazamo huu wa muda mrefu umezuia ushiriki wao katika nafasi za maamuzi, licha ya kuwepo kwa sera na sheria za kitaifa kama vile Sera ya Taifa ya Ardhi (1995), Sheria ya Ardhi ya Vijiji (1999), na Sheria ya Serikali za Mitaa (1982) zinazowatambua wanawake kuwa sehemu ya maamuzi na wamiliki halali wa ardhi. Tanzania pia imeridhia mikataba ya kikanda kama vile Itifaki ya Maputo na Ajenda ya AU 2063, ambazo zote zinasisitiza usawa wa kijinsia na haki za wanawake katika uongozi. Lakini utekelezaji wake, hasa katika ngazi ya jamii, bado unakabiliwa na changamoto nyingi kutoka kwenye mila na mitazamo hasi.



Baada ya kushiriki mafunzo ya uongozi mwaka 2024 kupitia UKIJANI, Pendo aliamua kuchukua hatua ya kuelimisha jamii. Hakukomea kwa wanawake pekee, bali aliwafuata pia wanaume ambao mara nyingi ndiyo wanaoamua hatma ya wake zao katika kushiriki siasa na uongozi. Aliwatembelea katika vijiwe vya kahawa, vilabu vya pombe, na viwanja vya mpira, akiwahamasisha wabadili mitazamo na kuwaunga mkono wanawake.

“Tuligundua kuwa hamasa kwa wanawake pekee haitoshi, kwa sababu wengi walikumbwa na vizuizi kutoka kwa waume zao. Tuligeukia wanaume ili wawe sehemu ya mabadiliko,” anaeleza Pendo.

Ushawishi wa Pendo ulianza kuzaa matunda. Mwanakijiji mmoja, Mzee Omary Salum, anakumbuka alivyoshangazwa na ujasiri wa Pendo:
“Sikuwahi kufikiria kuwa mwanamke angeweza kunikalia chini na kuniambia nimuunge mkono mke wangu kugombea. Lakini Pendo alikuja kwangu mwenyewe, alizungumza kwa upole lakini kwa msimamo. Alinifungua macho. Leo, mke wangu ni mjumbe wa kamati ya shule,” anasema kwa furaha.



Juhudi zake ziliwawezesha wanawake wengi kujitokeza kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2024. Tofauti na mwaka 2019, ambapo hakuna mwanamke aliyekuwa Mwenyekiti wa Kitongoji, mwaka 2024 wanawake wawili Neema Said Shila (kura 75) na Hadija Mohamed Dafi (kura 10) waliingia katika tano bora kwenye kura za maoni za nafasi ya uenyekiti wa kijiji cha Kikonge. Mwanamke mmoja aliyemhamasisha na kumpigia kampeni, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mabanda, ushindi mkubwa kwa wanawake wa eneo hilo.

Zaidi ya siasa, Pendo amekuwa nguzo ya mabadiliko katika maeneo ya elimu na huduma za kijamii. Kama Katibu wa UWT kata, anatumia nafasi yake kushawishi wanawake kuingia kwenye nafasi za maamuzi. Anasimamia ajenda za usawa wa kijinsia kama upatikanaji wa zahanati bora, afya ya mama na mtoto, chakula shuleni, ujenzi wa hosteli kwa ajili ya wasichana wa shule ya sekondari, na huduma za maji safi.

“Tukipata bweni moja kwa wasichana na lingine kwa wavulana, tutapunguza utoro na mimba za utotoni. Watoto watasoma bila hofu na kwa karibu na shule,” anasema Pendo.

Kupitia hamasa ya Pendo, wanawake wengi wameweza kupimiwa na kumiliki ardhi kwa mara ya kwanza. Alimshawishi Elisiana Mkumbo kuwania ujumbe wa Baraza la Ardhi la Kata, ambapo amesaidia kuelimisha wanawake juu ya haki ya umiliki wa ardhi.

“Awali wanawake wengi hawakujua umuhimu wa kumiliki ardhi. Waliona kuwa kama baba ameandikishwa inatosha. Sasa wengi wanatambua kuwa ni haki yao pia, na wameandikishwa kwenye hati miliki pamoja na waume zao,” Pendo anaongeza.

Baada ya mafunzo ya UKIJANI, Pendo na viongozi wenzake wa UWT wameanzisha ziara za shule kutoa elimu ya afya ya uzazi na kupinga ukatili wa kijinsia. Tayari wameanza kuona mabadiliko chanya ikiwa ni pamoja na kupungua kwa mimba za utotoni.

“Tuligundua kuwa viongozi wengi hawakuwa wanayapa kipaumbele masuala ya haki za wasichana. Sasa tumeanza ziara shuleni, na tunaanza kuona matokeo,” anasema Pendo.

Kupitia Halmashauri ya Kijiji, ambayo yeye pia ni mjumbe, wamekubaliana kuhakikisha huduma bora za jamii hasa maji, afya, na elimu zinapatikana kwa usawa, huku watoto wa kike wakipewa kipaumbele na ulinzi dhidi ya vitendo vya ukatili.

Hadithi ya Pendo Makala Mkumbo ni ushahidi kuwa uwezeshaji wa kweli huanza ngazi ya jamii. Ni ushuhuda kwamba kwa maarifa sahihi, ushawishi, na nia thabiti, wanawake wanaweza kuibuka kuwa viongozi wenye mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii zao. Kupitia UKIJANI, Pendo siyo tu anabadili mitazamo analea kizazi kipya cha wanawake viongozi Tanzania.