“Tamasha la Jinsia laja na mapendekezo haya’


“Tamasha la Jinsia laja na mapendekezo haya’

By Deogratius Temba

February 2, 2025


 Na Mwandishi wetu

 

Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), kwa kushirikiana na mashirika yanayotetea haki za wanawake na usawa wa jinsia nchini, Vituo vya Taarifa na Maarifa, na washiriki wa semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS), umefanya Tamasha la 7 la Jinsia ngazi ya Wilaya katika Viwanja vya Sabasaba, Wilaya ya Kondoa, Mkoani Dodoma.

 

Tamasha hili limeongozwa na mada kuu isemayo, “Dira Jumuishi ya 2050: Miaka 30 Baada ya Beijing Tujipange”, huku mada ndogo ndogo zikiangazia Miaka 30 ya Beijing: wako wapi wanawake viongozi; Rasilimali za taifa ziwanufaishe wananchi wa pembezoni; Harakati za kijamii na ushiriki wa makundi rika; Teknolojia, mabadiliko tabia nchi, masuala ya ukatili wa kijinsia;  na masuala ya kazi zenye ujira  na staha  kwa wanawake na vijana.

 

Tamasha hili limekutanisha zaidi ya washiriki 300 wanaojumuisha wananchi wa Kondoa, wanakituo cha Taarifa na Maarifa kata ya Haubi, wawakilishi kutoka serikalini ngazi ya mkoa, wilaya na Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa, wadau wa maendeleo, AZAKI, vikundi vya kijamii, vikiwemo vituo vya taarifa na maarifa kutoka Mtwara Vijijni, Kondoa Vijijini, Kishapu, Lindi, Same, Mwanga, Babati, Morogoro Vijijini, Gairo, Kinondoni, Ilala, na Ubungo,  na wanaharakati ambao wamekuwa bega kwa bega na TGNP katika kuchagiza usawa wa jinsia.

 

Tamasha lilifunguliwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule. Katika neno la ufunguzi alitambua mchango wa TGNP katika kuendeleza harakati za usawa wa jinsia tangu mwaka 1993 katika ngazi zote za kitaifa hadi katika ngazi za kijamii (kata) ili kuhakisha walengwa wanaohitaji elimu hii waipate, akitolea mfano kata ya Haubi ambayo alisema ni moja ya kata zinazohitaji sana elimu hiyo ya usawa wa kijinsia.

 

Kutoka na mijadala, midahalo na warsha zilizoendeshwa wakati wa Tamasha la Jinsia ngazi ya wilaya Kondoa, baadhi ya changamoto zilibainishwa na nyingine kutolewa ufafanuzi. Kutokana na changamoto hizo, washiriki wa tamasha walitoka na mapendekezo kadhaa ambayo ni pamoja na:

 

Iongeze bajeti kuboresha huduma za jamii ili ziweze kuwafikia wananchi, hususani waliopembezoni kwa urahisi na gharama nafuu au bure.  Kwa mfano; kuwaongezea mamlaka za maji bajeti za kuhakikisha kuwa maji yanasambazwa na yanapatikana wakati wote katika miundo mbinu iliyopo, hasa maeneo ya vijiji vya ndani ndani.  Bajeti ya maji bado haijapewa kipaumbele ni haizidi asilimia moja ya bajeti kuu.

 

Pia, halmashauri  zitenge fedha za kutosha za kutekeleza afua za kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa kundi rika balehe. Kuongeza uwekezaji wa kibajeti ili kuondoa kabisa vifo, vinavyozuilika, vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga na wale walio chini ya miaka mitano, gharama hizi za uzazi zinapaswa kutolewa bure kabisa. Bima ya afya, ambayo ni rahisi kupatikana na yenye gharama nafuu na inayoweza kulipia huduma bora za afya kwa kila mwananchi.

 

Kwa upande wa elimu ni uwekezaji katika kuweka mazingira bora ya elimu hususani kwa makundi maalumu ili wawaweze kupata elimu bila shida, kwa mfano mabweni kwa Watoto wanaoishi mbali na shule, miundo mbinu rafiki kwa Watoto wanaoishi na ulemavu, upatikanaji wa miundo mbinu na huduma rafiki kwa Watoto wa kike wakiwa katika hedhi; pia kuweka mazingira wezeshi kwa wasichana wanaorudi shuleni na Watoto wao baada ya kupata kujifungua.

 

Aidha, tunapenda serikali itenge bajeti kuwawezesha maafisa katika ngazi ya kata na vijiji kufikia vijiji mbalimbali kuwajengea wananchi, hususani wanawake uwezo na kuwasaidia kutatua changamoto zinazowakabili na kuwapa taarifa za fursa zilizopo na namna wanaweza kuzitumia ili kunufaika nazo. Mfano Maafisa Maendeleo ya jamii, Ustawi wa jamii, Ugani n.k

“ Tunatoa wito kwa wadau mbalimbali kusaidia wanawake kuingia katika nafasi za maamuzi na uongozi katika ngazi zote, kuanzia vitongoji, vijiji/mitaa, kata, wilaya hadi taifa ili kuongeza idadi ya wanawake katika ngazi za maamuzi na uongozi. Tunatarajia Wilaya hii ya Kondoa itakuwa ya mfano katika kuhakikisha kuwa wanawake wanaongezeka hadi kufikia 50/50 katika nafasi za mamuzi katika ngazi na sekta zote” alieleza sehemu ya mapendekezo hayo.

 

Pia ilipendekezwa kwamba serikali ya mkoa wa Dodoma iimarishe usimamizi wa utekelezaji wa agizo la serikali la matibabu bure kwa wanawake wanaojifungua kwa kutoa hizo namba na namna ya kutoa taarifa za ukiukwaji kwenye zahanati, vituo vya afya, hospoitali, na serkali za vijiji. “ ….Tunashauri halmashauri zitengeneze mwongozo wa maadili wa uendeshaji na usimamizi wa shughuli za baa, klabu n.k ili kuepuka kuendeleza vitendo vya udhalilishaji wa wanawake na wasichana vinavyofanyika katika maeneo hayo…”ilieleza sehemu ya mapendekezo ya tamasha wakati wa kufunga.

 

Pia ilipendekezwa kwamba serikali ishirikiane na wadau kuhakikisha kuwa wakulima wanapata elimu ya mabadiliko tabia nchi na teknolojia mbalimbali zinazosaidia katika kuzuia na kukabiliana na mabadiliko tabia nchi, ikiwemo kubainisha, kushirikisha, kujifunza na kutumia mbinu bunifu za wakulima wnaotumia kukabiliana na athari za mabadiliko tabia nchi na kuziendeleza.  Kwa mfano kwa upande wa kondoa, kutokana na ardhi kuwa imechoka, na ikiwekwa mbolea inahamishwa wakati wa mvua, wameanza kutumia teknolojia ya mbegu 9 na jembe la kondoa; na upande wa kata ya Mamire iliyoko Halmashauri ya Wilaya ya Babati, wamekuwa wakitumia kilimo ikolojia.