Nafasi ya mwanaume katika kujenga Jiji la Mungu; Kufuata nyayo za Mtakatifu Augustino


Nafasi ya mwanaume katika kujenga Jiji la Mungu; Kufuata nyayo za Mtakatifu Augustino

By Deogratius Temba

August 29, 2025

KUFUATA NYAYO ZA MT. AUGUSTINO

Nafasi ya mwanaume katika kujenga Jiji la Mungu; Kufuata nyayo za Mtakatifu Augustino

Utangulizi

Katika dunia ya sasa inayokabiliwa na changamoto nyingi za kijamii, kiroho, na kimaadili, mwanaume Mkristo anaalikwa kuishi maisha ya toba, upendo, na uongozi wa kiroho. Mtakatifu Augustino wa Hippo, mmoja wa watakatifu wenye ushawishi mkubwa katika historia ya Kanisa, anatoa mwanga wa kipekee kuhusu nafasi ya wanaume katika kulijenga Civitas Dei – yaani, Jiji la Mungu.
Makala hii imeandaliwa mahsusi kwa ajili ya wanaume katika familia, jumuiya, na katika parokia zetu ikilenga kuwasaidia kutafakari nafasi yao ya kiroho kwa kutumia mafundisho ya Mt. Augustino pamoja na Maandiko Matakatifu. Makala hii inatupa nafasi ya kumtafakari Mt. Augustino, Mwanaume mwenzetu na mwanaume aliyeishi maisha kama yetu tena katika mazingira ya kiafrika pia ambako ndiko ukristo uliko kwa kiasi kikubwa katika ulimwengu wa leo.

Mafundisho Kumi ya Tafakari kwa Wanaume, kwa kufuata nyayo za Mt. Augustino

1. Toba ya Kweli: Mwanzo wa Kujenga Jiji la Mungu

  • “Nilikuwa nimefungwa na minyororo ya mapenzi mabaya... Lakini 'sasa hivi' haikuwa sasa hivi.” (Confessions, VIII.12), katika Maandiko matakatifu, tunafundihswa: “Tubuni basi, mrejee mpate kufutwa dhambi zenu.” (Matendo 3:19). Mwanzo wa maisha mapya ya mwanaume ni toba ya kweli na kujikana nafsi. Toba humfungua mwanadamu katika uhuru wa kiroho.

2. Neema ya Mungu: Chanzo cha nguvu ya mwanaume

  • Mt. Augustino anasema“Atakayemwamini Mungu... atakuwa na matendo mema kwa neema Yake.” (On the Spirit and the Letter, 33), fundisho hili la Mt. Augustino linakaziwa na eno la Mungu linalosema; “Kwa maana mmeokolewa kwa neema... wala si kwa matendo.” (Waefeso 2:8-9). Tunahitaji neema ya Mungu kuishi maisha safi kama wanaume, Mwanaume wa Mungu anatambua kuwa nguvu ya kuishi kwa haki haitokani na juhudi zake binafsi bali ni zawadi ya neema ya Mungu.

3. Upendo: Msingi wa maisha ya kikristo

  • Katika suala la Upendo, Mt. Augustino anatufunidhsa kwamba,  “Kama haufanyi kazi ya kujenga upendo... bado hujayafahamu Maandiko.” (On Christian Doctrine, I.36)
  • Fundisho hili la Mt. Augustino linajengwa katika misingi ya neno la Mungu’ “Upendo huvumilia yote... haupungui nguvu kamwe.” (1 Wakorintho 13:7-8), Upendo kwa Mungu na jirani ni msingi wa maisha ya mwanaume anayeijenga jamii ya Mungu – jamii inayosimikwa katika haki, huruma, na mshikamano.

4. Uongozi wa Kiroho: Wito asilia kwa mwanaume

  • Mt. Augustino, anatufundisha kwamba “Jiji la Mungu linajengwa na wale wanaopenda Mungu hadi kujikana nafsi zao.” (City of God, XIX.14)
  • Biblia: “Mume ni kichwa cha mke kama Kristo alivyo kichwa cha Kanisa.” (Waefeso 5:23). Uongozi wa mwanaume unapaswa kuwa mfano wa Kristo – si wa kutawala kwa nguvu, mabavu au kukandamiza wengine, bali wa kuhudumu kwa upendo, hekima, na kujitolea.

5. Ndoa Takatifu: Sakramenti ya Kujitoa

  • “Ndoa ni nzuri kwa sababu huzaa watoto na kuimarisha jamii.” (On the Good of Marriage, 9) funisho hili linaimarishwa na maandiko matakatifu yanayosema  “Mungu alimuumba mwanamume na mwanamke... watakuwa mwili mmoja.” (Mwanzo 2:24)
  • Ndoa ni agano la kiroho linalomwita mwanaume kuwa mwaminifu, mlinzi, na kiongozi wa familia yake kwa mapendo ya kweli.

6. Maisha ya Kujitolea: njia ya utakatifu

  • Mt. Augustino anasema- “Furaha ya kweli ni kumpenda na kumiliki Mungu.” (Of the Morals of the Catholic Church, 3). “Kama mtu yeyote anataka kunifuata... na ajikane mwenyewe.” (Luka 9:23)
  • Maisha ya kujitolea ni kiini cha safari ya mwanaume wa Mungu. Kwa kujikana na kujitoa kwa ajili ya Mungu na wengine, mwanaume huingia kwenye utakatifu. Sadaka kubwa ya mwanaume kujitoa ni pamoja na kuipigania familia aliyopewa na Mungu. Wale walioko katika familia ni zawadi ambayo Mungu amempatia mwanaume, kujitoa kwake kwaajili yao kutampa utakatifu.

7. Vita vya Ndani: Kupambana na tamaa za dunia

  • Augustino anatufundisha “Bwana, nifanye kuwa safi... lakini si sasa hivi.” (Confessions, VIII). “Roho hutamani yaliyo ya Mungu, lakini mwili hutamani yaliyo ya dunia.” (Wagalatia 5:17)
  • Mwanaume wa kiroho hutambua mapambano ya ndani yanayoendelea kila siku, na humtegemea Roho Mtakatifu kwa ushindi.

8. Utunzaji wa familia: Kiongozi na mlezi wa maadili

  • Augustino anatufunidha kwamba: “Familia ni jiji dogo la Mungu.” (Muhtasari wa mafundisho yake ya kijamii). “Yule asiyeweza kuiongoza nyumba yake vema, atawezaje kuliongoza Kanisa la Mungu?” (1 Timotheo 3:5)
  • Familia ni mahali pa kwanza pa kulea maadili. Mwanaume anaalikwa kuwa kiongozi mwenye upendo, asiyeacha jukumu la kiroho au malezi kwa mke wake pekee.

9. Maombi na Tafakari: uhusiano wa kiroho na Mungu

  • Augustino anatufundisha: “Umetuumba kwa ajili yako, Ee Mungu, na moyo wetu hautatulika mpaka upate pumziko kwako.” (Confessions, I.1). “Ombeni bila kukoma.” (1 Wathesalonike 5:17)
  • Maombi na tafakari ni pumzi ya kiroho. Bila hayo, mwanaume anakauka kiroho na kushindwa katika vita vya maisha. Askari mzuri ni yule anayejinadaa na kuandaa silaha za mapigano. Mawanaume anahitaji sala ili aweze kushinda mapambano aliyo nayo katika maisha

10. Mwanaume Mpya: Kiumbe Kipya katika Kristo

  • Nukuu ya Augustino: “Mabadiliko ya kweli huanza pale mtu anapokutana na Upendo wa Mungu.” (Confessions). “Tazama, mambo ya kale yamepita; tazama, yamekuwa mapya.” (2 Wakorintho 5:17)
  • Kila mwanaume anayekutana na Kristo hupewa maisha mapya – si kwa jina tu, bali kwa matendo yanayoonyesha toba na upendo wa Mungu.

Hitimisho na Sala

Ee Bwana wa Majeshi, tunakuomba uwainue wanaume katika kizazi hiki wawe viongozi wa kiroho, walimu wa haki, na wapenzi wa familia zao. Utupe wauame wote nguvu, ujasiri, moyo wa kujitoa kwa unyenyekevu katika kujenga jiji la Mungu katika familia zetu, utupe njia sahihi na za haki za kujipatia riziki zetu ili tuwajibike kikamilifu. Tunakuomba utujaze kwa neema Yako, utuongoze kwa hekima Yako, na utufundishe upendo wa kweli ili tushiriki kwa dhati katika kulijenga Jiji Lako hapa duniani. Tunaomba hayo kwa njia ya Bweana wetu Yesu Kristo. Amina.

MT. AUGUSTINO WA HIPPO-UTUOMBEE!

Tafakari hii imeandaliwa na Na Deogratius Temba

Rafiki wa Mt. Augustino

deojkt@gmail.com