Wananchi wa Msigani wajipanga kutumia ‘Kilichopo Mikononi Mwao’ kuleta maendeleo


Wananchi wa Msigani wajipanga kutumia  ‘Kilichopo Mikononi Mwao’ kuleta maendeleo

By Deogratius Temba

April 30, 2025

Na Mwandishi Wetu

Kuanzia tarehe 19 hadi 30 Aprili 2025, Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) uliendesha mafunzo ya mchakato wa Utafiti wa Shirikishi – Participatory Action Research  (PAR) katika Kata ya Msigani, Manispaa ya Ubungo. Mafunzo haya yalilenga kuwawezesha wananchi, hasa wanawake, kuwa mstari wa mbele katika maendeleo ya jamii zao kwa kutumia mbinu ya Maendeleo jumuishi yanayotokana na rasilimali za ndani- Asset-Based Led Community Developement (ABCD).

Mafunzo yaliongozwa na Mraghibishaji wa TGNP, Deogratius Temba, ambaye alitumia mbinu shirikishi kuwawezesha  wanajamii kutambua rasilimali walizonazo na namna ya kuzitumia kuleta maendeleo. Akisisitiza falsafa ya “Tumia kilichopo kupata usichokuwanacho” iliyoasisiwa na Padre Moses Coady, Temba alisema: “Tunapozingatia misingi ya ABCD, tunawasaidia wananchi kutambua kuwa wao wenyewe ni sehemu ya suluhisho. Wanapofahamu rasilimali walizonazo, wanapata nguvu ya kuchukua hatua badala ya kusubiri misaada kutoka nje.”

Katika mafunzo hayo, Temba aliwaeleza washiriki kuhusu dira, dhima na mikakati ya TGNP, ikiwa ni pamoja na mzunguko wa harakati ya Haki za wanawake na Usawa wa Kijinsia (IMBC). Pia alielezea kwa kina dhana ya PAR na mbinu ya Triple A inayojumuisha hatua tatu muhimu: Uibuaji (Assess), Uchambuzi (Analyse), na Utekelezaji (Action). Washiriki walijifunza namna ya kutumia hatua hizi kutambua changamoto katika jamii zao, kuchambua sababu na kupanga hatua za pamoja za kutatua changamoto hizo kwa kutumia rasilimali zilizopo.

Mafunzo yalihusisha pia matumizi ya Mfumo wa Pentagoni (R-5) kwa kutambua aina tano za rasilimali ndani ya jamii: watu, maliasili, kijamii, kiuchumi, na kitamaduni. Washiriki waligundua kuwa walimu, vijana, mafundi, ardhi, miti, mito, vikundi vya kina mama, vyama vya kijirani, biashara ndogondogo, mifugo, nyimbo za kitamaduni na mila mbalimbali ni utajiri mkubwa wa jamii ambao unaweza kutumika kama nguzo ya maendeleo. Rasilimali hizi ziliwekwa kwenye mpango wa pamoja wa utekelezaji wa maendeleo ya jamii.

Mary Luhambati, mmoja wa washiriki, alisema: “Katika vitu nilivyojifunza ni kutambua na kuchambua hizi rasilimali tano zilizoko kwenye jamii. Kwangu hii ilikuwa muhimu sana. Mbinu hizi za misingi ya ABCD zimenifungua akili yangu—kwamba tunaweza kutumia tulichonacho kupata kile ambacho hatuna. Pia nimeweza kuunganisha jitihada za jamii na zile ambazo serikali imekuwa ikizifanya. Baada ya mafunzo haya, tutashirikiana zaidi na serikali yetu kuleta mabadiliko makubwa sana katika jamii yetu.”

Doreen Nanyaro, mshiriki mwingine kutoka Msigani, aliongeza: “Tumejifunza kuwa hatuhitaji kusubiri mtu kutoka nje aje kutuletea maendeleo. Tayari tunavyo vya kutosha kuanza kubadilisha jamii yetu—tulichohitaji ni mabadiliko ya mtazamo.”

Mbinu hizi zimeonesha mafanikio makubwa kwa jamii ya Msigani. Kupitia ushirikiano wa TGNP na Taasisi ya Coady kutoka Canada kupitia Mradi wa Engage, jamii zimepata uelewa na nguvu ya kuongoza maendeleo yao kwa mtazamo wa usawa wa kijinsia.

Msigani sasa ni mfano hai wa jinsi jamii inaweza kubadilika na kusonga mbele kwa kutambua vipaumbele vyao, kutumia rasilimali zilizopo, na kushirikiana kwa pamoja—bila kusubiri msaada kutoka nje.