"Zainab Hamis Husein: Uongozi na Ardhi kwa Maendeleo ya Kiuchumi"


"Zainab Hamis Husein: Uongozi na Ardhi kwa Maendeleo ya Kiuchumi"

By Deogratius Temba

March 26, 2025


 

Na Deogratius Koyanga

Zainab Hamis Husein-Sekuka ni mmoja wa wanufaika wa Mradi wa UKIJANI unaotekelezwa na asasi ya Helvetas Tanzania katika mkoa wa Singida, wilaya ya Ikungi. Anasema, "Licha ya jamii inayozunguka familia yetu kuamini kwamba mwanamke hana haki ya kumiliki ardhi, familia yangu ilikubaliana kumilikisha ardhi kwangu, jambo ambalo limeleta mabadiliko makubwa katika ndoa yetu na jamii yetu."

Mumewe, Mzee Ramadhani Mohamed, maarufu kama Kitifui, ambaye awali alimiliki mashamba zaidi ya kumi, anasema, "Nimepata elimu, nimeelemika, na niliona manufaa ya kumilikisha mke wangu ardhi kwa jina lake. Hii imetusaidia kuondoa migogoro ya familia na kuongeza amani nyumbani." Alielewa umuhimu wa kumilikisha ardhi kwa jina la Zainab baada ya kushiriki katika mafunzo ya Mradi wa UKIJANI na kusema, "Hii ni fursa ya kipekee. Nimeona umuhimu wa kuweka vizuri umiliki wetu wa ardhi ili kuondoa migogoro, hasa kwa wanawake, hasa tunapokuwa hatupo."


Zainab anasema, "Hili shamba lilikuwa la mume wangu, lakini baada ya mafunzo ya uongozi na usimamizi wa rasilimali kupitia Mradi wa UKIJANI, nilielewa umuhimu wa kumiliki ardhi na faida zake. Nilimfundisha mume wangu, na alikubali kumiliki ardhi hiyo kwa jina langu na kutoa sehemu kwa watoto wetu."

Mradi wa UKIJANI umeleta mabadiliko makubwa katika familia ya Zainab. Mzee Ramadhani anasema, "Mimi ni mnufaika wa elimu inayotolewa na mradi wa UKIJANI. Nimejifunza mengi kupitia mke wangu na watoto wangu, na sasa hapa kwetu kumekuwa kama Kituo kikubwa cha kujifunzia." Zainab na mumewe wamefanikiwa kufanya shughuli za kilimo na ufugaji kwa kutumia mbinu za ikolojia, wakiwa na mifugo ya maziwa, kuku wa kienyeji, na uzalishaji wa mkaa mbadala. Mradi huo umeongeza kipato cha familia na kuwasaidia kujenga nyumba kubwa ya kisasa. Ramadhani anasema, "Tumeboresha nyumba yetu kwa kupiga lipu, kuweka bati mpya, na kuweka umeme. Huu ni mafanikio makubwa kwa familia yetu."

Zainab ameweza kutimiza malengo yake ya kusaidia wanawake katika jamii yake. "Nilifanya kampeni kwa wanawake 62, na kati yao, mmoja aligombea uenyekiti wa vitongoji, na wengine 8 waligombea nafasi za ujumbe wa serikali ya kijiji na kushinda," anasema Zainab, akionyesha mafanikio ya mradi katika kuhamasisha wanawake kushiriki katika uongozi.

Hadithi ya Zainab na mumewe ni mfano halisi wa jinsi elimu, fursa za kiuchumi, na usimamizi wa rasilimali ulivyoleta mabadiliko katika familia yao. "Mradi wa UKIJANI umeleta ustawi wa kiuchumi, kuboresha mahusiano ya familia, na kuongeza usawa katika umiliki wa rasilimali," anasema Zainab, akiwa na matumaini ya kuendelea kuwa mfano wa mafanikio kwa wanawake wengine.